Ingia / Jisajili

Bernard Mukasa

Mfahamu Bernard Mukasa, mtunzi wa nyimbo za Kanisa Katoliki. Kutoka Jimbo la Dar es Salaam Parokia ya Makuburi

Maelezo zaidi

Idadi ya nyimbo SMN: 184 > Zitazame

Jimbo analofanya utume: Dar es Salaam

Parokia anayofanya utume: Makuburi

Namba ya simu: +255 655 670 785

Soma Historia na maelezo yake hapa

Wasiliana na mtunzi kwa email:


Historia / Maelezo

Tumsifu Yesu Kristo. 
 
Bernard Mwombeki Mukasa anaimba sauti ya nne, kwaya ya Mt. Kizito Parokia ya Mwenyeheri Anuarite - Makuburi, Dar Es Salaam.
 
Mwaka huu 2016 ni mwaka wa 36 tangu alipoanza kuimba kwaya miaka 36 iliyopita, akiwa na umri wa miaka mitatu. Kwa neema ya Mungu ameandika nyimbo kadhaa, yapata 1,500 hivi mpaka sasa. Kati ya Hizo, karibu 700 zimerekodiwa katika albamu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
 
Katika utume wa uimbaji, Mungu amemjalia takribani tuzo tano, ikiwemo tuzo ya KUMBUKUMBU YA KARDINALI RUGAMBWA YA MTUNZI WA WIMBO BORA WA KANISA KATOLIKI (Mwaka 2003), na TUZO YA MUZIKI YA KILIMANJARO (KILIMANJARO MUSIC AWARD) YA MTUNZI BORA WA MUZIKI NCHINI TANZANIA (mwaka 2005).
 
Bernard Mukasa amebahatika kuwa mwasisi halisi wa kwaya moja mpaka sasa, Kwaya ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo (BMW) Parokia ya Biharamulo, Jimbo la Rulenge - Ngara (1995), na baadaye kutunukiwa hadhi ya kuwa "Baba wa Kwaya" wa kwaya hiyo mwaka 2005.
 
Tena, Kwa Neema ya Mungu, alibahatika kuasisi mifumo mitatu muhimu kwa utume wa uimbaji wa leo nchi Tanzania na Afrika Mashariki: 
 
 1. Mfumo wa utoaji sauti zenye nguvu na angavu, unaoitwa jina maarufu siku hizi "sauti za kupuliza", mwaka 2002.
   
 2. Mfumo wa utawala wa Kwaya wa kisekta, unaofanya kwaya iongozwe kwa kushirikisha kamati kadhaa hasa kamati kuu, kamati ya ufundi na Liturjia, ya Fedha na Mipango, ya Nidhamu na Mahusiano, na ya Sare na Unadhifu, mwaka 2000.
   
 3. Mfumo wa utunzi unaobeba ghani asili kabisa ya Kitanzania ikichanganya na asili ya katikati mwa afrika, mwaka 2000. Hata hivyo mfumo huu umezua mjadala mkubwa wa wanazuoni wa muziki wa kanisa. Wapo wanaouona kuwa unaamsha uhai wa ibada na uhai wa nyimbo, na wapo wanaouona kuwa unaathiri uchaji katika hasa pale unapotumika kwenye ibada. Bernard Mukasa anaamini mwisho wa mjdala huu mzito utakuwa ni kupatikana kwa mfumo wa kati ambao unamfanya Mungu atukuzwe na kuheshimiwa, lakini wale wanaomtukuza wanajisikia kulifurahia tendo hilo la kumtukuza Mungu vizuri zaidi.
 
Miaka mine na nusu iliyopita, Bernard Mukasa aliasisi kundi la facebook la wadau wa utume wa uimbaji liitwalo Fr. G.F.KAYETTA ambalo linakua kwa kasi na limesimama kama kiungo muhimu kwa kuwafanya waimbaji wafahamiane na kuwasiliana kwa urahisi zaidi bila kujali mipaka ya kijiografia. Kundi hili limevuka mipaka ya Tanzania, na sasa lina wanachama kutoka Tanzania, Kenya, Kongo DR, Malawi, Msumbiji, Madagasca, Peru, na wachache toka nchi za Ulaya.  Kundi hili, limeasisi vuguvugu/mchakato wa kuanzishwa kwa shirikisho la Utume wa uimbaji Tanzania, ambao bado unaendelea kwa kujaribu kuwashirikisha wadau muhimu ndani ya kanisa.
 
Aidha, kundi hili limezaa mtoto muhimu yaani tovuti ya nyimbo za kanisa za kiswahili, www.swahilimusicnotes.com, miongoni mwa matunda mengine kadhaa. Na baada ya kuunganishwa na Kayetta group na kuwa na mawasiliano ya pamoja, wadau mbalimbali wa utume wa uimbaji wameweza hatimaye kutokea humo kuwasiliana na kuunda makundi mengine kadhaa ya mitandao ya jamii yenye malengo maalumu zaidi ndani ya utume wa uimbaji. Miongoni mwa makundi hayo ni CATHOLIC MUSICIANS ORGANISATION (CMO), CATHOLIC TANZANIA ORGANISTS, MFUKO WAKUSAIDIANA WA WANAKAYETA, nk. Haya yote ni matunda chanya au uzao mwema wa kuasisiwa kwa kundi la Fr. Kayetta Group.
 
Mwaka 2006, Bernard Mukasa aliasisi SIKU YA KUOMBEA UTUME WA UIMBAJI jimboni Dar Es Salaam sambamba na chama cha walimu wa kwaya Jimbo kuu la Dar Es Salaam, akishirikiana kwa karibu sana na Ndg. Richard Mloka. Hata hivyo mwaka uliofuata siku hiyo haikuadhimishwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuondoka Dar Es Salaam kwa Mukasa mwenyewe huku jambo likiwa bado changa. Baada ya miaka kadhaa, uongozi wa Shikwaka Jimbo kuu la Dar Es Salaam ukafufua wazo hilo na kuanzisha siku ya walimu wa Jimbo kuu la Dar Es salaam, na kufanya mpaka leo tukio hili liwe limeadhimishwa kwa mwaka wa nne sasa ingawa huko nyuma kuna miaka ilirukwa. Wazo hili linazidi kukua na kupokeleka kama kiungo muhimu cha ushirikiano wa walimu wa kwaya nchini.
 
Mwaka 2008, Bernard Mukasa alijaliwa kuasisi TAMASHA LA KUOMBEA UTUME WA UIMBAJI Jimbo la Sumbawanga ambalo limeendelea kuadhimishwa kila mwaka mwezi January, sambamba na kutunga SALA YA KUOMBEA UTUME WA UIMBAJI ambayo iko katika sauti za nota, hivyo huimbwa.
 
Na baadaye, mwaka 2013, Mukasa aliasisi Tamasha maarufu lijulikanalo kama TAMASHA LA YESU NI MWEMA (TYM) linaloendeshwa na kwaya ya Mt. Kizito Makuburi, linalofanyika mara moja kila mwaka.
 
Mpaka sasa Bernard Mukasa ameshiriki na kurekodi kanda za kusikiliza (audio albums) zaidi ya 80, na za kutazama (Video albums) 3, zote zikiwa zimefanikiwa sana sokoni. Miongoni mwa albamu alizosimamia maandalizi yake ni pamoja na:
 
 1. Siri ya Moyo wangu – Kizito Makuburi
   
 2. Silaha ya Mapambano – Kizito Makuburi
   
 3. Mungu Yule – Kizito Makuburi
   
 4. Nyumba ya Roho – Kizito Makuburi
   
 5. Mbingu Zahubiri – Cecilia Ifakara
   
 6. Acheni Kukata Tamaa – Maurus Misa ya kwanza Kurasini
   
 7. Bwana Ameweza – Stephano Kipawa
   
 8. Mungu – Ledokoska Dodoma
   
 9. Siri ya mafanikio – Denisi Sumbawanga
   
 10. Asante Mungu – Josefu Ruanda Mbeya
   
 11. Mlipuko wa Sifa – Yuda Thadei Mbeya
 
Miongoni mwa kwaya alizowahi kuziendeshea mafunzo maalumu ya uimbaji na zikapiga hatua kubwa za wazi ni pamoja na Kizito Makuburi, Ledokoska Dodoma, Cecilia Ifakara, Yuda Thadei Mbeya Mjini, Watakatifu Wote Kiluvya, na Familia Takatifu ya kanisa kuu la Mt. Josefu Dar Es Salaam.
 
Kwaya alizowahi kuimbia ni Pamoja na:
 
 1. Kwaya ya malaika (kwaya ya watoto misa ya jioni) - Parokia ya Biharamulo,
   
 2. Kwaya ya Mt. Cecilia - Parokia ya Biharamulo
   
 3. Kwaya ya YCS Tabora Boys
   
 4. BMW Parokia ya Biharamulo
   
 5. Kwaya ya Mt. Fransisco Exaviery - Parokia ya Chang'ombe Dsm
   
 6. Kwaya ya Mt. Denisi Sebugwao - Parokia ya Kristo Mfalme Sumbawanga
   
 7. Kwaya ya Mt. Joseph Mfanyakazi - Parokia ya Ruanda, Mbeya (Alikokutana na Changamoto ngumu sana katika utume wake, kuliko hata na huwa hafurahii hata kuzikumbuka wala kuzisimulia).
   
 8. Kwaya ya Mt. Kizito (KMK) - Parokia ya Makuburi DSM, ambako amekuwa mwanakwaya kwa miaka 17 sasa, na ndiko sehemu kubwa kabisa ya mafanikio yake katika utume wa uimbaji ilikopatikana. Hii ndiyo kwaya yake RASMI anayoihesabu kama KWAYA YA MAISHA YAKE.