Ingia / Jisajili

Tenzi za Kiswahili

Na Ronald Nakaka: 

Ndugu Terence Vusile Silonda na mimi tulijadili wazo moja ambalo tuliona ni muhimu kuliwasilisha kwenu watumishi. Tuliona ni vyema tuakaanzisha kwenye Swahilimusicnotes.com (SMN) category mpya ya "Swahili Hymns" au "Tenzi za Kiswahili", ambayo itahusu nyimbo aina ya hymns.

 

Kwa lugha ya kigeni, hymn ni aina ya tenzi ya kusifu au kuabudu ambayo maneno yake ni ya ushairi wa kutunga au kutoka kwenye zaburi. Kwa uzoefu wangu, nyimbo hizi zipo nyingi, hasa zamani na zimekusanywa katika Kitabu maarufu cha Mkusanyiko wa Nyimbo na Kwa wenzetu Waprotestanti, katika Kitabu cha "Tenzi za Rohoni", lakini nyimbo hizi --kama nyimbo nyingine maridadi katika tamaduni mbalimbali za Kikristo-- zimeweza kukubalika na madhehebu mengi ya Kikristo na zimekuwa zikiimbwa, ingawa kuna tofauti kidogo katika tafsiri au arrangement ya muziki. Nyimbo maarufu za mlengo huu ni kama "What a friend we have in Jesus" (Yesu ni rafiki yetu), "All hail the power of Jesus' Name " (Msifuni Yesu mwokozi), "And can it be" ( Ni Upendo).

 

Hivyo, malengo mahsusi yakurasa huo katika SMN ni kama ifuatavyo:

 

  1. Kuzikusanya tenzi hizo za kale, pamoja na nyingine zilizokuwapo tayari katika vitabu vya Mkusanyiko na Tenzi za Rohoni
  2. Kuchochea utunzi mpya wa nyimbo hizo, ambazo zitatungwa kwa tafakuri nzito, ubunifu wa kishairi, usahihi wa kitheolojia, pamoja na utamu wa kimuziki. Nyimbo hizo ziweze kudumu kwa karne nyingi zijazo, na kuwa urithi kwa Kanisa, kama ambavyo sisi tumerithishwa na waliotutangulia.
  3. Kuchochea matumizi ya nyimbo hizo katika ibada za misa na mikusanyiko mbalimbali ya waumini.
  4. Kuchapisha kitabu kipya cha tenzi, za watunzi wapya na zile za zamani katika mpangilio mpya, n.k

 

Ninatambua kuwa kuna watu wamekwisha kutunga nyimbo za aina hii, na huenda tayari zipo kwenye SMN katika category ya "Nyimbo za Tafakari" au "Zaburi". Tukiafikiana, tutasaidiana kuzipeleka nyimbo hizo kwenye kundi hili jipya ndani ya SMN, huku tukipokea na nyingine nyingi zitakazotungwa.

Tunaomba mawazo yenu. Ni sisi, Terence na Nakaka.


Tumsifu Yesu Kristo.

UPDATE:

 

Category Hiyo Tayari imeanzishwa. Tafadhali tembelea hapa > http://www.swahilimusicnotes.com/category/tenzi-za-kiswahili