Mfahamu Bernard Mukasa, mtunzi wa nyimbo za Kanisa Katoliki. Kutoka Jimbo la Dar es Salaam Parokia ya Makuburi
Idadi ya nyimbo SMN: 239 > Zitazame
Jimbo analofanya utume: Dar es Salaam
Parokia anayofanya utume: Makuburi
Namba ya simu: +255 655 670 785
Soma Historia na maelezo yake hapaWasiliana na mtunzi kwa email:
Mwezi Februari mwaka 2006, Bernard Mukasa aliasisi siku ya walimu wa kwaya wa
Jimbo kuu la Dar Es Salaam, iliyopewa jina la Tamasha la utume wa uimbaji,
ambayo iliwaalika na kuwashirikisha wanakwaya wote hata wasiokuwa walimu.
Katika kuasisiwa kwa siku hii, ilikusudiwa kuwadhimishwa kila mwaka Jumamosi ya
mwisho kabla ya Kwaresma. Katika kuasisi siku hii, alisaidiwa kwa karibu sana na
Mwl. Richard Mloka na Dismas Malya. Lengo kuu lilikuwa kuwaunganisha pamoja
walimu wa kwaya wa Dar Es Salaam na polepole wa Tanzania nzima ili hatimaye
kuasisi chama cha walimu wa kwaya katoliki Tanzania, kusudi kuboresha
mahusiano mema kati yao, hatimaye kuleta umoja ambao baadaye ungeweza
kurahisisha uundwaji wa shirikisho la kwaya la kitaifa.
Hata hivyo siku ya Walimu haikuadhimishwa mwaka uliofuata baada ya muasisi wake kuhamia nje ya Dar Es Salaam kikazi. Lakini kwa bahati njema, mwaka 2008 shirikisho la kwaya la Jimbo hilo (SHIKWAKA) liliiboresha siku hiyo na sasa ikawa inaandaliwa na SHIKWAKA kila Jumamosi moja kabla ya Pentekoste.
Mwaka huo huo 2008, Bernard Mukasa aliasisi Tamasha la kila mwaka la Utume wa Uimbaji kwa Jimbo la Sumbawanga sambamba na sala maalumu ya kuombea utume wa uimbaji ambayo inaimbwa kwa muziki wake maalumu, ambavyo kwa pamoja vilizinduliwa rasmi na Baba Askofu Damiano Kyaruzi. Ingawa mwaka uliofuata Bernard Mukasa alihamia jimbo jingine tena kikazi, tamasha hili limeendelea kuadhimishwa kila mwaka mwezi Januari jimboni Sumbawanga.
Mwaka 2010, Bernard Mukasa aliasisi kundi la mtandao la facebook la wadau wa utume wa uimbaji liitwalo Fr. G.F.KAYETTA ambalo lilikua kwa kasi na kusimama kama kiungo muhimu cha kuwafanya waimbaji wafahamiane na kuwasiliana kwa urahisi zaidi bila kujali mipaka ya kijiografia. Kundi hili lilivuka mipaka ya Tanzania, likawa na wanachama kutoka Tanzania, Kenya, Kongo DR, Malawi, Msumbiji, Madagasca, Peru, na wachache toka nchi za Ulaya. Kundi hili, liliasisi vuguvugu la kuanzishwa kwa shirikisho la Utume wa uimbaji Tanzania, vuguvugu ambalo halikufanikiwa kufikia mwisho huko mtandaoni kwa sababu ya tofauti nyingi za kimitazamo, mpaka miaka sita baadaye pale ambapo vuguvugu hilo lilienea na kufika masikioni mwa mababa wa kanisa, nao wakaamua kulirasimisha vuguvugu hilo kuwa mchakato rasmi wa kikanisa chini ya Baraza la Maaskofu Tanzania. Mchakato huu hatimaye ndiyo uliozaa Utume wa kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA) mwaka 2018, na Bernard Mukasa akateuliwa na Raisi wa Baraza la Maaskofu kuwa mratibu wa kwanza wa Utume huo.
Aidha, kundi hili la mtandaoni la Fr. Kayeta lilizaa tunda jingine muhimu ambalo ni tovuti ya nyimbo za kanisa za kiswahili, www.swahilimusicnotes.com, miongoni mwa matunda mengine kadhaa. Mtaalamu mwanzilishi wa tovuti hii, Mwana- 4 Kayetta Terence Vusille Silonda, baadaye kwa hiari yake aliikabidhi tovuti hii kwa Baraza la Maaskofu na sasa imekuwa mali ya kanisa kwa ajili ya kuuhudumia utume wa kwaya.
Na baada ya kuunganishwa na Kayetta group na kuwa na mawasiliano ya pamoja, wadau mbalimbali wa utume wa uimbaji waliweza hatimaye kutokea humo kuwasiliana na kuunda makundi mengine kadhaa ya mitandao ya jamii yenye malengo mahsusi zaidi ndani ya utume wa uimbaji. Miongoni mwa makundi hayo ni CATHOLIC MUSICIANS ORGANISATION (CMO), CATHOLIC TANZANIA ORGANISTS, MFUKO WAKUSAIDIANA WA WANAKAYETA, na mengine mengi. Haya yote ni matunda chanya au uzao mwema wa kuasisiwa kwa kundi la Fr. Kayetta Group.
Baadaye, mwaka 2013, Bernard Mukasa aliasisi Tamasha maarufu la kila mwaka lijulikanalo kama TAMASHA LA YESU NI MWEMA (TYM) lililoendeshwa na kwaya ya Mt. Kizito Makuburi kwa miaka 4 ya kwanza. Baadaye kwaya hii ilijihisi kukosa utaalamu wa kutosha wa kuliandaa na kuliendesha, na ukakubaliana na muasisi wa tamasha aendelee kuliendesha mwenyewe. Hivyo kuanzia mwaka 2017 Tamasha hili linamilikiwa na kuendeshwa na kampuni yake binafsi inayojishughulisha na masoko, kampuni ya NIMEONJA PENDO COMMUNICATIONS LTD (NPC).
Mpaka sasa Bernard Mukasa ameshiriki na kurekodi albamu zaidi ya 100 zikiwemo za kusikiliza (audio albums) na za kutazama (Video albums). Miongoni mwa albamu alizosimamia maandalizi yake ni pamoja na:
Aidha, Bernard Mukasa ameendesha mafunzo maalumu kwa kwaya mbalimbali
na kuzijengea mapinduzi makubwa ya kiumbaji na kimfumo. Baadhi ya kwaya
hizo baada ya hapo zilipiga hatua kubwa na mpaka sasa zimebaki kuwa
miongoni mwa kwaya za mfano. Hizi ni pamoja na Mt. Kizito Makuburi (KMK),
Ledokoska - K’ndege Dodoma (BMTL), John Paul - II Mbeya Mjini (JMC), Mt.
Cecilia Makuburi, nk.
Kwaya alizowahi kuimbia ni Pamoja na:
Kimuziki, Bernard Mukasa alianza safari yake kwa kufundishwa muziki nyumbani
akiwa na umri mdogo kabisa alipokuwa darasa la kwanza. Mwalimu wake wa
kwanza wa Muziki ni kaka yake ambaye kwa sasa ni Padri, Pd. Faustine
Binamungu Mukasa s.j, ambaye kwa kiasi fulani alishirikiana na kaka mkubwa
zaidi (mzaliwa wa kwanza wa wazazi wake), Mwalimu Patrick Mukasa. Baadaye
Mukasa alipojiunga na masomo ya Sekondari katika shule ya sekondari ya
wavulana Tabora alijiendeleza kimuziki kwa kujiunga na somo la muziki hapo
shuleni chini ya mwalimu Kanyabwoya. Wakati huo pia alikuwa akisaidiwa
masomo ya ziada ya muziki toka kwa wanafunzi waliokuwa wamemtangulia
vidato, hasa hasa Inoocent Kanubo Mukuyuli, Nyachuma Miyaga na zaidi sana
Ndg. Edward Samsoni Kidola.
Hata hivyo, Mukasa hakudumu sana na darasa la Mwl. Kanyabwoya baada ya kuona kama mtaala husika uko nyuma ya kiwango cha ujuzi alichokuwa amekwishakipata, akaamua kutumia nafasi hiyo kusoma sayansi ya kilimo. Jambo hili halikumfurahisha sana Mwl. Kanyabwoya ambaye ndiye alikuwa mkuu wa idara ya muziki, kiasi cha kumtenga Mukasa na fursa mbalimbali za idara hiyo. Kwa bahati njema, kipaji cha Mukasa kilitambulika kwa gwiji wa muziki wa kanisa Pd. Luis Malema Mwanampepo aliyekuwa anafundisha katika seminari kuu ya Kipalapala, ambaye alimpa Mukasa fursa ya kuwa anakwenda kuhudhuria darasa lake kila wikiendi. Kifupi, darasa kuu la muziki kwa Mukasa ni Seminari kuu ya Kipalapala – Tabora kwa Pd. Malema, ingawa yeye hakusoma katika seminari hiyo. Darasa hili lilisaidiwa sana na chama maalumu cha Muziki cha jimbo la Tabora (TAEMO) ambacho wakati huo kilikuwa kiliongozwa na mwenyekiti Frt. John Damasen Zilimu na katibu Frt. Ponsianus Kibobela (wote walikuwa mapadri baadaye).
Baada ya kutoka Tabora, Mukasa aliendelea kujiendeleza kwa nadhalia ya muziki kwa vyanzo mbalimbali, lakini alibahatika kupata kozi maalumu ya vitendo katika chuo cha Chiriku Musiconsult kilichokuwa kikimilikiwa kwa pamoja na waalimu watatu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (Dionizi Mbilinyi, Sabinus Komba na John Mgandu). Mukasa alijiunga na kozi hizi kwa kugharamiwa na kwaya ya Mt. Kizito Makuburi ili akajifunze upigaji wa kinanda kwa kuwa kwa wakati huo kwaya hiyo haikuwa na mpiga kinanda wa uhakika, lakini yeye alipofika huko akabadilisha kozi kimya kimya na kusoma kozi tatu tofauti kabisa ambazo yeye aliamini ndizo hasa zitamjenga kuchangia chachu yenye upekee katika fani hiyo.
Sababu nyingine iliyomsukuma Mukasa kubadili kozi ni kwa kuwa aligundua kwamba hizo kozi tatu zikiunganishwa pamoja gharama yake ni sawa na ile ya kozi moja tu ya kinanda, kwa sababu watu wengi walikuwa hawajiungi nazo hivyo hazikuwa na soko sana. Kozi ya kwanza ilikuwa ya kanuni na mbinu za uimbaji (Choral Techniques), ya pili ilikuwa ualimu wa kwaya na uimbishaji (Choir mastering), na ya tatu ikawa utiribu (Professional conducting.)
Zaidi ya muziki, Mukasa amekuwa mtu mwenye kupenda kuandika vitabu mbalimbali vya dini, ingawa hajafanya vya kutosha katika eneo hilo. Mpaka Januari 2020 Mukasa ameandika vitabu vitatu ambavyo bado havijachapishwa na kusambazwa (Mungu Yule, Ongoko, na Utume wa Uimbaji), na ameandika kitabu kimoja kilichochapishwa na kusambazwa (Gusaneni Majeraha).
Mbali na kuwa mratibu wa utume wa kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA) nafasi iliyompa tiketi ya kuwa mjumbe wa Halmashauri ya Walei ya Taifa, Mukasa pia amekuwa mjumbe wa Halmashauri ya Walei ya Jimbo kuu la Dar Es Salaam na Parokia ya Makuburi kwa tiketi ya kuwa katibu wa Halmashauri ya Walei ya Parokia, kifupi katibu wa Parokia.
Baada ya kuajiriwa katika taasisi kadhaa, hatimaye Mukasa amejiajiri kama muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ukuzaji Masoko inayoitwa NIMEONJA PENDO COMMUNICATIOS (NPC) ambayo pamoja na mambo mengine inajishughulisha na uwakala wa masoko, ushauri elekezi wa kimasoko, uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, usambazaji na ukuzaji wa bidhaa za wengine, vyombo vya habari, usambazaji na ukuzaji wa kazi za muziki, nk. Biashara za NPC zinaweza kufikiwa kwa namba ya simu 0768670785 na barua pepe karibu@nimeonjapendo.co.tz
Miongoni mwa malengo ya hivi karibuni ya kiuchumi ya Mukasa ni pamoja na mkakati wa kuanzisha gazeti litakaloitwa Nimeonja Pendo, Kituo cha Redio na cha TV kwa jina hilo hilo la Nimeonja Pendo.
Kifamilia, Bernard Mukasa amefunga ndoa na mwalimu mwenzake wa kwaya, Matilder Sendwa, na wamejaliwa kupata watoto wanne; Victoria, Vinny, Vivian na Vince. Kwa bahati, watoto wao pia wana uelekeo wa utume wa uimbaji. Wanaimba kama wazazi wao, na tayari mmojawao ni mpiga kinanda. Katika kukuza vipaji vya watoto wao, Bernard Mukasa na Mkewe huimba katika kwaya ya familia inayoundwa na wao na watoto wao, ambayo ilianza ikiitwa TRIPLE V, na baadaye ikaitwa QUADRI’V baada ya kuzaliwa kwa Vince.
Tumsifu Yesu Kristo.